Pages

Tuesday, 28 May 2013

HISTORIA YA KARAGWE KWA MUHTASARI


Utangulizi
Tunapozungumzia historia ya watu wa mahali fulani hatuna budi kuzungumzia Jiografia ya sehemu husika, hali ya hewa na mazingira , wakazi wake ,uoto wa asili ,utamaduni wao ,utawala ,mawasialiano na uchumi . Lengo la kutafuta na kuifahamu vyema historia ya watu wa Karagwe ni la msingi sana. Lengo kuu ni kuandaa mazingira ya watu mbalimbali  ili waweze kuielewa vyema  historia ya Karagwe, kukusanya na kuzihifadhi zana na kumbukumbu za kimila na jadi ambazo katika siku za karibuni zinaelekea kuanza  kupotea. Makala hii itachambua kwa kina historia ya kabila la Wanyambo ambao kwa asili wanatoka Wilaya ya Karagwe Mkoani Kagera.
   

CHIMBUKO LA KARAGWE NA WATU WAKE (WANYAMBO).

Jina “ Karagwe “ kutokana na simulizi za wazee wetu mbali mbali na watafiti wa historia ya Karagwe  kama ( Katoke 1975; 162) inaelezwa kwamba  jina hili linatokana na kilima (angalia kielelezo hapa chini) kinachopatikana Kusini Magharibi ya Makao makuu ya wilaya  ya Karagwe ,kwenye kijiji cha Kandegesho ,kata ya Nyakakika ambacho mtawala ( Omukama ) wa kwanza alifanya kafara ya kwanza. Taarifa zilizopo mtawala huyo alijulikana kwa jina la Nono ya Malija kutoka ukoo wa Basiita. Na kwamba kumbukumbu hii ya “Karagwe ka Nono “inatokana na ukweli kuwa Nono alikuwa mtawala wa mwisho wa wenyeji asilia wa Karagwe kabla ya kuondolewa madarakani na Omukama Ruhinda mtoto wa Wamara. Inasemekana kwamba Nono son of Marija alikabidhi madaraka yake bila ya misukosuko wala mapigano ya aina yoyote kwa ajili ya kuokoa watu wake waliokuwa wanakabiliwa na wimbi la njaa. Kwa kifupi hii ndio kumbukumbu yake na chimbuko la historia ya jina Karagwe.


Hiki ndicho kilima kiitwacho na kijulikanacho kama “ Karagwe “ 
Kielelezo ”B”

Mlima Karagwe unapakana na ziwa linaloitwa na wenyeji kuwa “ ziwa Kitete “ lenye wanyama aina ya kiboko wengi ambalo pia linapakana na hifadhi ya wanyama pori ya Kimisi. Kielelezo “C”

Cory (1949; 18) anaendelea kueleza kuwa “Ruhinda alipofika Karagwe kutoka kusini alimkuta mtawala mwenyeji aliyekuwa akiitwa Nono son of Malija wa ukoo wa Basiita. Nono hakushindwa katika vita bali alidanganywa na ujanja wa Ruhinda “. Tafiti hii inashabihiana na simulizi za wazee wengi wa Karagwe na nchi jirani  kuwa Wasiita kutokana na njaa kali iliyokuwepo wakati huo waliuza ngoma ya utawala kwa wahinda /Ruhinda na kupewa ulezi  kwa ajili ya chakula na kuanzia wakati huo wakawa chini ya utawala wa Abahinda /Ruhinda . Ruhinda alijenga Boma lake eneo la Bwehange nchi iliyo kusini ya ziwa lililoitwa Speke “The little Windemere” na baadae kuhamia Bweranyange, mahali palipo karibu na uwanda wa juu penye mteremko wa vilima vinavyozunguka ziwa. Hapa ndipo watawala wote waliopotawalishwa hadi walipofika wadachi.

Birigitta Farelius 2008 katika utafiti wake anasema “ Popote unapokuta ng’ombe machungani katika Afrika ya Mashariki macho huvutiwa sana na ndege weupe (white cow herons ) wajulikanao kama Nyange Nyange , nao watu wa Karagwe huwaita Enyange ,wakifuatana na ng’ombe na kazi yao kubwa husaidia kudonoa kupe na wadudu wanashambulia mifugo. Ndege hawa hupendwa na wenyeji kutokana na tabia yao ya kutoa huduma kwa mifugo yao tofauti na ndege wengine waharibifu wanaoshambulia mazao, hawa hawana madhara ya aina yoyote. Makao makuu ya Omukama Rumanyika wa Karagwe yalikuwa katikati ya makundi ya wafugaji na kulikuwepo na ndege hawa wengi  na hivyo kupewa jina la Bweranyange kutokana na ndege hawa kupenda kutanda eneo hili muda wote “.

Na hili linathibitishwa na simulizi za wenyeji wa eneo hili ambao wengi walikuwa wafugaji, na sisi pia tunalazimka kukubaliana na matokeo ya utafiti huu unaonyesha chimbuko la jina la Bweranyange wakiwa na maana sehemu safi na nyeupe (makao makuu ya mtawala wao) kutonana na umaarufu wa ndege hawa.

Ni kutokana na ukweli huu wenyeji walitunga wimbo maarufu wa kumsifia mtawala wao ,na kwa mtawala halisi na makini kama alivyokuwa Omukama Rumanyika alitakiwa kuwa na roho nyeupe ya upendo kwa watu wake na wimbo huu ulikuwa unaimbwa popote pale alipotembelea na kulala . Wimbo huu uliwaasa na kuwaonya wananchi kuwa wasikivu, wastaarabu, wenye kufuata kanuni, sheria na kutokuwa wasumbufu kwa mgeni wao aliyewatembelea.
Mtayomba mwalirwa enyange ……….
Mtayomba …………………………….
Ne enyange ti nyange …………………
N’omwana ‘womuntu ……………..
Mtayomba …………………………..
Leba no omwana wo omuntu ……….
Mtayomba ………………………….

Hapa ndipo ilipokuwa makao makuu ya watawalala wa Karagwe, Bweranyange ambayo yamebaki magofu.

Kielelezo “D” Mabaki ya majengo ya Bweranyange

“The little windermere lake  “  Kama lilivyobatizwa na John Hanings Speke linavyonekakana toka makao makuu ya Bweranyange

Kielelezo “E”

Taarifa za Utafiti huu unashabihiana kwa karibu sana na ule wa Bwana HALLEY katika kitabu chake cha “An African Survey “ ukurasa 23/24 “ akielezea kwamba kaskazini magharibi ya ziwa Victoria ‘’ Watu wa makabila ya Waganda ,Wanyankole , Watoro ,Wanyoro na makabila manane ya wilaya ya Bukoba katika Tanganyika na Ruanda (Nchi ya udhamini ya ubeligiji) ni mchanganyiko wa makabila ya wenyeji wakulima wabantu na makabila ya wafugaji wa kihima toka kaskazini ambao yasadikiwa kwamba yalizishambulia nchi hizo zama za miaka mia tatu iliyopita na kuwashinda wenyeji wake . Katika falme hizi wafugaji wa ng’ombe waitwao wahima mpaka sasa ni jamaa wa watawala”.

Wakaazi wote wa Karagwe walimtegemea Omukama kwa ushauri na ulinzi. Alitoa maelekezo katika masuala yote muhimu kuhusu maeneo ya Karagwe. Pamoja na kuwepo kwa makabila lukuki Wilayani Karagwe; hatimaye iliwezekana kuanzishwa kwa Umoja wa Karagwe ambao uliwezesha makabila yote kukaa pamoja na kujadili masuala mbalimbali ya kijamii.

Kuanzishwa umoja wa Karagwe na utawala (Kingship) uliwezekana kwa wakati huo kutokana na mambo makuu yafuatayo;
Kuongezeka ka idadi ya watu kutokana na mapinduzi ya kilimo
Uongozi bora uliooneshwa na mtawala “Omukakama”  na
Ongezeko la wahamiaji kutoka Bunyoro ambapo walikuwa wanalazimika kukimbia mapigano na uvamizi wa watu toka maeneo ya kaskazini.

Kuwepo kwa mchanganyiko wa makabila mbali mbali katika Karagwe unaanzia karne ya 18 ambapo Stanley (1876) anaripoti kuwa “in Karagwe there were Wanyambo, Wanyarwanda, Wasuwi, Wanyamwezi, Arabs, and Swahili,  as observed at the court of King Rumanyika .

Taarifa hii inatuonyesha kuwa Karagwe na Kyerwa toka zamani hadi leo imekuwa ni kisiwa cha utulivu na amani. Ni kutokana na kuwepo kwa utulivu na amani hii, kumekuwepo na mwingiliano wa makabila mbali mbali. Aidha;  kutokana na sababu mbali mbali zilizowakabili majirani kama ukame, njaa ,matatizo ya kiuchumi na kisiasa  , na wakati mwingine mapigano ya koo na kabila yamesababisha watu wengi kutoka makabila tajwa  kuhamia Karagwe . Hivyo, Karagwe na Kyerwa kwa sasa pamoja wenyeji wake (Wanyambo) wanaishi na watu wa makabila mbali mbali kutoka ndani ya nchi na wengine kutoka nchi jirani za Rwanda, Burundi na Uganda.

Leo hii ukitembelea kijiji cha Kafuro katika kata ya Nyabiyonza utaona mwembe mkubwa ulipandwa na kuachwa na wafanyabiashara wa kiaarabu waliofika Karagwe katika karne ya 18 kwa ajili ya biashara ya kubadilisha pembe za ndovu na bidhaa nyingine.

Huu mti wa mwembe uliopandwa na Waaarabu katika karne ya 18 katika kijiji cha Kafuro

Kielelezo “F”
Taarifa zilizopo zinaonyesha kuwa wakati Omukama Rumanyika Orushongo anaingia madarakani, Karagwe ilikuwa tayari imekua kiuchumi kiasi ambacho wafanyabishara toka maeneo ya mbali walikuwa wameanza kuingia Karagwe wakifanya biashara ya meno ya tembo, mazao ya chuma (Iron products) kama vile visu, majembe na vitu vingine wakibadilishana na bidhaa waliyoleta toka maeneo waliyotoka.

Mwishoni mwa karne ya 18 na mwanzoni mwa karne ya 19, habari za kushamili
kwa Karagwe kutokana na biashara zilikuwa zimesambaa sehemu mbalimbali  za nchi ya Tanganyika pamoja na nchi za jirani za Rwanda, Kongo, Uganda, Burundi na hata nchi za Falme za Kiarabu. Wakati huo Karagwe ilikuwa imekwishatembelewa na wajasiliamali toka Unyamwezini na Usumbwa ambao walileta chumvi toka Uvinza na chuma toka Katanga (nchini Kongo) .

Hili linathibitishwa na msemo wa kinyambo wa muda mrefu unaosema “Omwonyo ngunula, chonka Omushumbwa nanunka”kwa kiswahili maana yake ni kwamba chunvi yao ni tamu pamoja na kwamba wachuuzi wenyewe wanatoa harufu mbaya ya jasho tokana na safari yao ndefu.


Inaaminika pia kwamba Wanyamwezi walifika Karagwe wakiwa watu wa kwanza kufanya biashara na kwamba walileta chumvi, visu, pilipili,na matunda kama vile  maembe, machungwa na mtama kabla ya Waarabu kuingia ambao walijenga Kituo chao maeneo ya  Kafuro na Kitengule.

Shughuli za Kisiasa, biashara na watu wa mbali (Tabora na Pwani) ilianzisha na kujenga mahusiano mazuri na watawala (Abakama) wa Karagwe, kiasi kwamba Omukama Rumanyika I wakati huo alilazimika kumteua msadidizi wake « Kiyango kya Mpiga Ifumula Bikungu «  kuwa Balozi wake katika tawala za jirani zake ambaye wakati huo alikuwa akisafiri kati ya Bweranyange, Buganda, Bunyoro, na Tabora.Kazi kubwa ya mteule Kiyango kya Mpiga Ifumula Bikungu ambaye unaweza kumuita kama balozi ilikuwa ni kufanya mawasiliano na kuimarisha kati ya Mtemi  Rumanyika na  watawala wa sehemu hizo.  Balozi huyu alionekana kupata sifa nyingi za utendaji kazi, sifa ambayo ilitolewa wazi wazi na wageni kama Captain  John Hanings Speke na Grant (katika kitabu chaek kiitwacho The jouney of discovery of River Nile ) walipozuru Karagwe. Ilikuwa ni kupitia kwake wageni hawa waliweza kupokelewa na watawala ikiwa ni pamoja na Omukama Rumanyika bila matatizo yeyote.

Haya yanathibitishwa na mzee wetu marehemu Profesor Katoke (1975;55) ambaye aliandika “ Ikumbukwe kuwa Speke na Grant walipata upinzani mkubwa katika sehemu zingine za Kigoma na Tabora ambapo waliingia bila kuwasiliana na Kiyango, waliweza kuzuiliwa kwa muda na wakati mwingine kutozwa ushuru mkubwa na watawala wa maeneo hayo wakiwa safarini   kuelekea Karagwe “. Hii inathibitisha umuhimu wa Balozi huyo Kiyango cha Mpiga Rufumura Bikungu.

3.JE , WANYAMBO NI WATU WA AINA GANI?

Neno “Wanyambo “hakuna mtu mwenye uhakika na mwenye kutoa maelezo mazuri ya kuridhisha kuwa linatokana na nini au lina maana gani. Katoke (1975;7 ) anaeleza katika utafiti wake kuwa zipo simulizi mbali mbali mbali kuwa wanyambo wanatokana na kizazi cha “Kanyambo” ,mtoto wa “ Ruhanga “ambaye alitumwa kuanzisha nchi ya Karagwe toka Bunyoro .Hivyo ,watoto na vizazi vyake ndani ya Karagwe kuitwa wanyambo , na kwamba kabila hili limegawanyika katika makundi ya wakulima na wafugaji. Pia , wapo watu wanatoa simulizi huko Bunyoro (nchini Uganda ) kuwa mababu zao walizaliwa kutoka Karagwe . Aidha, ipo aina ya ndizi asilia inaitwa “enyambo” na ng’ombe asilia mwenye pembe fupi aitwaye “ente ye enyambo”

Lakini, watafiti wengine kama Birgitta (2008) na wengineo wanaeleza kuwa neno “Wanyambo “linatokana na jamii ya “Abaragwe” waliohamia Ankore toka Karagwe miaka mingi iliyopita. Inaaminika kuwa watu hawa ambao walikuwa wabantu waliongea lugha ya “Oluragwe” na kwamba lugha hii imepotea kutokana na mwingiliano na mchanganyiko wa lugha toka katika  makabila mbali mbali yaliyoingia Karagwe na kutengeneza kinyambo cha sasa kinachozungumzwa na wanyambo wa Karagwe .

Ni kutokana na kukinzana kwa maelezo ya tafiti hizi tunapenda kuamini kuwa hakuna mtu mwenye maelezo mazuri ndani ya karagwe au nje Karagwe mwenye kuelezea bila ya mashaka yoyote kuhusu  neno “Wanyambo” linatokana na nini au chimbuko lake halisi ni nini.

Hata hivyo hatuna budi kukubaliana na  Birgita Farelius (2008; 35-38 ) katika utafiti wake ambaye  anasema yafuatayo nami bila kupotosha nanukuu “ To the South of Ankole, the people of Karagwe in the former Tanganyika were placed under the heading of the “Haya” in for example Audrey Richard’s Volume on East African Chiefs (1959;174-194) .The Bahaya proper were basically fishing people whom the first Europeans had found along the Lake Victoria .However, it was recognized that the Inhabitants of Karagwe ,the Banyambo were not to be “ considered as pure Bahaya because of their strong Rundi element ,also in their language “ (Cory 1949;13). In principle Karagwe can be  termed as free state from Bukoba and is separated from the Bukoba area “in terms of geology ,climate ,vegetation ,population density and economy” (Schmidt 1978;12) quoting the 1988 population census that , the figure for Karagwe was 292.589 people ,while Bukoba Urban and Rural including Muleba had 665.412 inhabitants.

Moreover, In the Kingdom of Buhaya power evolved around the ownership of cultivated land; while in Karagwe power evolved around cattle ownership (Katoke 1975;36 , Anacleth and Ndagala 1981; 154) . In the Nyarubanja land tenure system in the Buhaya, the kings could confiscate banana plantations and then confer them in his favourities or relatives .And the original occupants, who could have been clan heads, were allowed to stay on as tenants, the landlords enjoying the tribute from their labour. Again, this system did not exist in Karagwe (see for example Cory and Hartnoll 1945;123-124 and Ishumi 1971;724).

Naye Bishop J. Kibira (1974; 11) as quoted by Birgita (2008 ) says, for the purpose of colonial administrative expediency, Karagwe was categorized as part of Buhaya “tribe “under Bukoba district, although their socio –economic structures, their culture and their language differ. In fact Buhaya and Karagwe have been characterized as “almost two different countries in one region”.

The Luhaya spoken by the Bahaya and the Runyambo of the Banyambo in Karagwe are treated as dialects of one language belonging to Rutara group of Great lakes Bantu Speakers.  But, Bashungwa (1988) , a Mnyambo linguistic in his research does not support this conclusion, but suggests that there is a closer affinity between Runyambo and Runyankole than Runyambo and Ruhaya .

Moreover, Karagwe and Buhaya traditionally had different political systems; the kingdom of Karagwe ,which the colonialists found in place ,had more in common with Nkole than with the Buhaya Kingdoms.

 Kwa tafsri yangu napenda kuamini kwamba wakoloni kwa sababu za kiutawala waliunganisha (Wanyambo) toka Karagwe na (Wahaya) toka Bukoba na wote kuitwa “Wahaya” ili kurahisisha utawala wao walipoingia nchini Tanzania. Lakini ,ni ukweli usipingikika kwamba Wanyambo wanaopatikana katika wilaya ya Karagwe na wahaya toka Bukoba wanatofautiana sana kutokana na asili yao , shughuli za kiuchumi ,kijamii , Mila na desturi , mazingira , na lugha zao kama tafiti hapo juu zinavyoeleza . Aidha, Kinyambo kutokana na tafiti hapo juu kinashabihiana zaidi na Kinyankole kuliko kihaya.

Hata hivyo ,jamii ya watu wanaoishi katika wilaya ya Karagwe kwa sasa ina mchanganyiko wa makabila mbali mbali kama vile wanyambo ,wahaya ,wasubi ,wanyarwandwa ,wanyankole ,warundi ,wazinza ,wahangaza n.k .Kwa mbali na historia wanyambo ni watu wakarimu sana na wanaopenda kuishi na watu toka makabila tofauti bila ubaguzi.

UTAWALA  NA WATAWALA  WA Karagwe

Kama ilivyokwishaelezwa hapo juu mtawala wa kwanza wa Karagwe alijulikana kwa jina la Nono ya Malija , Ruhinda alipofika Karagwe kutoka kusini alimkuta mtawala huyu mwenyeji  ambaye alilazimika kuachia madaraka yake na kumpisha Omukama  Ruhinda ili kuokoa watu wake waliokuwa wanakabiliwa na njaa wakati huo.

Ruhinda baadae alijenga Boma lake eneo la Bwehange eneo lililopo  kusini mwa  ziwa Kajunju ambalo baade lililobatizwa na Bwana Speke “The little Windemere” akiwa na maana ya kuwa lilifanana sana na ziwa Windemere linalopatrikna nchini Uingereza ,na baadae Omukama Ruhinda aliweza kuhamia Bweranyange, mahali palipo karibu na uwanda wa juu penye mtelemko wa vilima vinavyozunguka ziwa hili .Hapa ndipo watawala wote waliofuatia waliopotawalishwa hadi walipofika wadachi. Inaelezwa kuwa hakuna msukosuko mkubwa uliotokea wakati wa utawala wa Omukama Ruhinda, na inasemakana alitawala watu wake kwa haki na utulivu kwa miaka mingi.

Omukama Ruhinda alirithiwa na mwane Ntare mwaka 1800, wakati huo kulitokea mashambulio ya Wanyoro katika Karagwe na kwa vile Omukama Ntare alikuwa bado mdogo alikimbia na mama yake,  akabaki wakili wake ambaye pia aliuawa na Wanyoro.  Baadae wanyoro walishambuliwa  na ugonjwa mbaya ambao unasemekana kuwa ulitokana na uchawi wa Ntale aliopewa na Mfalme wa Uha (Buha –Kigoma)  na wakati anarudi na mama hakukuta mnyoro hata mmoja kwani wale ambao hawakufa walikimbia kwa woga. 

Mfalme Ntare alifuatiwa na Ruhinda VI ambaye maisha yake yalikuwa marefu sana hata mwisho watu kuamini kwamba hatakufa. Omukama Ruhinda VI aliamua kujiua mwenyewe ili kumpisha mwanae Ndagara ili atawale , Ndagara alikuwa shujaa wa vita alipigana vita na Kiziba ,Kyamtwala na Ihangiro .Hakuna ushahidi wa kutosha lakini mara zote simulizi za wazee wanyambo husema Ushindi katika vita hii ulikuwa wa kwao!!.

Ndagara alikufa mwaka 1855 na mwanae Rumanyika alitawazwa kuwa mfalme wa Karagwe kabla ya kukutana na Bwana Speke mwaka 1861.

Watawala wengine waliotawala Karagwe walikuwa kama ifuatavyo;

Ruhinda I
Ntare
Ruhinda II
1550 Ntare II
1575  Ruhinda III
1595 Ntare III
1620 Ruhinda IV
1645  Ntare IV
1675 Ruhinda V
1700 Rusatira
1725 Mehiga
1750 Kalemera
1775 Ntare V (Kiitabanyoro)
1795 Ruhinda Orushongo
1820 Ndagala I
1853 Rumanyika I
1883 Kayenje Kalemela
1886 Ndagala II
1893 Ntare VI
1916 D.Rumanyika II
1939 B.I.Ruhinda VII –The last Muhinda ruler of Karagwe
1963 End of political power of traditional rulers in Tanzania.

Chifu David Rumanyika II


Omukama Bernado Itogo Ruhinda VII aliyetawala kuanzia mwaka 1939
  
5.    TARATIBU ZA KUMWEKA MTEMI (OMUKAMA ) MADARAKANI.

Kabla sherehe ya kutawazwa Omukama kuanza ilikuwa ni jukumu la mmoja wa watu wa ukoo wa ”Abasindi” kuandaa ,kusafisha na kuhakikisha zana zote zilizotakiwa kutumika katika sherehe za kutawaza mtawala zinawekwa tayari. Wakati ukifika Omukama mtarajiwa alikaa katika viganja vya mmoja katika watu wanaotoka katika ukoo wa ”Abakaraza” . Huyu mara zote  alikaa karibu na kiti cha Omukama ambacho kilikuwa kimetengenezwa kwa shaba ( kigoda hiki kilichukuliwa na wajerumani  hadi leo hii hakijawahi kurudishwa). Sherehe hizi za kumtawaza mfalume ziliendeshwa na mjumbe toka ukoo wa Abasindi. Alichukua fito ndogo (Emiziyo) na kumkabidhi Omukama mtarajiwa  ambaye aliombwa kupiga ngoma.

Kitendo cha kupiga ngoma ikatoa sauti kiliashiria kuwa sasa ni mtawala rasmi mwenye uwezo wa kuongoza na kutoa maamuzi ya nchi iliyo mikononi mwake , anakuwa na uwezo wa kuita watu kwake kwa kutumia ngoma  na kuwaamrisha kufanya lile atakalowambia .

Aidha ,mtawala alikabidhiwa upinde na mishare , mkuki na ngao ikiwa ishara kwamba analo jukumu la kulinda na kutetea kiti chake na watu wake. Baada ya kupiga ngoma na kukabidhiwa zana za ulinzi ,alikaa katika kigoda cha utawala kilichokuwa kimetengezwa kwa shaba tupu (Copper Royal stool).

 Wakati haya yakitendeka mtu toka ukoo wa ”Omukaraza ” atakuwa amesimama kushuhudia  Mtawala mpya akitawazwa na kula kiapo cha ofisi mpya.  Huyu angeweza kufananishwa kama mama au baba wa ubatizo katika ubatizo wa kikristo (i.e Christian baptism).

Baada ya kutawazwa Omukama alipelekwa mtoni  sehemu iliyojulikana kama ”Mwogamarinzi” ili  kumalizia sehemu ya mwisho ya sherehe za kumweka madarakani mtawala .Sehemu hii ipo katika pango kando kando ya ziwa lijulikanalo kama Lweru rwa Bijunju. Alichukua mkuki wake na kuvaa sandals (Enkeito) na ngozi ya mnyama. Alipofika katika eneo hili alizamishwa kwenye maji kwa ajili ya utakaso na kusafishwa , wakati wote eneo hili takatifu lilitunzwa na  mtu mmoja tu toka ukoo wa ”Abasabya” ambao walikuwa wakiishi eneo hilo wakilitunza .

Wakati akioga /anasafishwa mtu mmoja toka ukoo wa ”Abasabya” aliuwawa na damu yake kuwekwa kwenye mto wa maji haya yanayotumika kumuosha Omukama .

Damu hii iliyomwagika katika mto huu wakati mtawala huyu anatakaswa ilikuwa na maana zifuatazo;-
Kumsafisha Omukana awe safi (mtakatifu)
Kudhihirisha kuwa Omukama kuwa sasa ana uwezo wa kutoa hukumu ya kifo kama ataona kuna sababu za msingi za kufanya hivyo.
 Baada ya hapa sherehe ziliendelea siku nzima na jioni Omukama na watu wote waliongozana wakirudi Ikulu ambapo alikuja kufanya mambo ya mwisho kwa siku hiyo . Alipofika ikulu yake alisimama mbele ya nyumba aliyojulikana kama ”Kajumilo” , kama utaratibu ulivyokuwa alitumia nafasi hii kama sehemu ya ibada ya kuombea nchi yake amani , kuwakemea na  kuwalaani watawala wa nchi jirani wenye mahusiano mabaya na nchi yake . Pia , aliwaombea majirani zake wenye mahusiano mema na nchi yake ya  Karagwe kuendeleza mahusiano mema na utawala wake .

Katika hatua nyingine ya mwisho katika kukamilisha utaratibu  , Omukama alipewa mbegu na watu wa ukoo wa ”Abaitila” ambazo alizitupa kuonyesha  kila kona ya Karagwe wakati huo akitoa maneno ya baraka .Aliombea nchi yake neema ya kupata mvua za kutosha  , rutuba ya ardhi na ya utu, amani na mshikamano. Katika maombi haya alisaidiwa na mtu maalum ambaye alimpatia dawa iliyosadikiwa kuwa na nguvu maalum inayomsaidia Omukama katika maombi yake. Baada ya kukamilisha ratiba hii Omukama aliondoka na kurudi katika Ikulu yake kwa mapumziko .


 MAHAKAMA ZA JADI – KARAGWE .

Mahakama ni chombo muhimu kwa serikali yoyote hapa duniani . Kazi kubwa ya mahakama ni kuhakikisha kwamba sheria za utawala /nchi zinafuatwa na kutekelezwa ipasavyo. Kila Mahakama ina wajibu wa kuhakikisha kuwa kila mwananchi anapata haki yake ilivyo kisheria. Vivyo hivyo nao wananchi hawana budi kutekeleza wajibu wao kisheria ,maana hakuna haki bila ya wajibu.

Utawala wa watu wa Karagwe ulikuwa na mahakama ya jadi na utaratibu wake wa kuhakikisha kila mtu anapatiwa haki yake .Aidha ,kabla ya ujio wa wakoloni malalamiko na madai mbali mbali yalisikilizwa na kutolewa uamuzi kupitia mahakama za jadi. Utaratibu huu ulikuwepo hata wakati wa mtawala wa kwanza wa Karagwe aiyeitwa Nono ya Malija .

Kuondolewa kwa utawala wa asili wa wabantu na kuingia kwa utawala wa Bahima kulileta utaratibu mpya wa kutatua migogoro na mashauri katika jamii . Baadhi ya migogoro iliyokuwa inatatuliwa ndani ya koo na mfumo wa vijiji ilibadilishwa na kuelekezwa kwa mtawala mpya, kwani utawala mpya ulikuwa umehaidi kutenda haki na kutoa ulinzi kwa kila mwananchi.

MAHAKAMA ZA JADI ZILIVYOFANYA KAZI .

Ni kwamba mashauri madogo madogo yalikuwa yanatatuliwa na wanaukoo au wanakijiji husika. Kwa mfano mashauri mgogooro wa  mali kati ya wanafamilia yalitatuliwa na baba , na kama mgogoro unahusu ukoo ingewezekana kusikilizwa na kutatuliwa na na mkuu wa ukoo.

Iwapo shauri ,kwa upande mwingine ,linahusisha watu wa koo mbili tofauti ,lakini toka kijiji kimoja ,shauri hili lilikuwa lilisikilizwa na kutolewa uamuzi na viongozi wa kijiji (Abakungu) ambao walikuwa wakichaguliwa kwa kuzingatia uwezo na busara zao.

Shauri lililowahusisha Wahima na Wanyambo asilia lilisikilizwa na mwakilishi wa Omukama aliyejulikana kama “Omukungu” kiongozi wa kijiji au Omulagilwa (msaidizi wa Omukungu). Vyombo vyote hivi vilikuwa na uwezo wa kusikiliza na kutatua mashauri ya madai tu.

Mashauri ya jinai yalikuwa yanasikilizwa na Omukama mwenyewe au mtoto wake aliyemchagua mwenyewe kufanya kazi hiyo kwa niaba yake.

Adhabu zilitolewa kulingana na mazingira ya hali ya kila kosa na  ukubwa wa kosa lenyewe .Iwapo kosa linahusu mauaji mali ya marehemu walipewa ndugu zake, mkosaji alitobolewa /kutolewa macho au mshtakiwa kutupwa kwenye korongo refu kwenye mwamba lililokuwa jirani na makao makuu Bweranyange lililojulikana kama “Rwebagira “.  Rwebagira ilimaanisha sehemu inayochinja yenyewe, au mahali pa kutekelezea huku ya kifo kwa mkosaji aliyekuwa amehukumiwa adhabu ya kifo.

Sehemu hizi za kutekelezea hukumu ya kifo “Rwebagira” zikuwa zimetengwa kwa jinsi , ilikuwepo sehemu ya kunyongea wanaume na ile ya kunyongea wanawake waliopatikana na makosa ya jinai na wasichana waliopata mimba nje ya ndoa.

Kesi za kujeruhi kwa kutumia mkuki, upinde na mishale, mali za mshtakiwa zilitaifishwa na nusu kuchukuliwa na OMUKAMA. Mwanaume alikuwa anaruhusiwa tu kuua mwanaume yoyote akimfumania akifanya zinaa na mke wake maana zinaa ilisemekana na kuaminiwa kuwa ingeleta mikosi kwa mhusika mwenyewe na nchi kwa ujumla. Watuhumiwa waliopatikana na makosa ya wizi walipewa adhabu ya kukatwa mikono yao ili wasirudie na iwe fundisho kwa wengine ambao walikuwa na mawazo ya aina hiyo.

Amri ya kuua mtu ilitolewa na Omukama pekee. Aidha , ukoo wa Abayango ni ukoo pekee ambao viongozi wake wangeweza kubatilisha amri iliyotolewa na Omukama . Birgitta Farelius (2008; 178) anathibitisha hili katika utafiti wake anaposema ” There was only one clan in Karagwe ,whose officials had the power to reverse an order given by the King .If the king gives an order to kill some one nobody else but an official of the Bayango clan could ask the king to forgive the victim.” Na hii ilitokana na imani kwamba ngoma ya utawala mzimu wake ulikuwa “Muyango” , hivyo aliwathamini Wayango kuwa sehemu ya utawala wake .

Aidha , Watuhumiwa wote wakati wakisubiri hukumu zao walipelekwa na kuhifadhiwa katika kisiwa kilichojulikana kama “Kazingaine “ kinachopatikana katika Ziwa Kajunju karibu na yaliyokuwa makao makuu ya Chifu (Omukama) Bweranyange .
Mtuhumiwa alipohukumiwa adhabu ya Kifo alipelekwa na kurushwa akiwa amefungwa kamba kwenye mwamba mkali ujulikanao “Rwebagira “ ili afe .

Chini ni picha ya mwamba huu kama unavyoonekana hadi sasa.

 Huu ndio mwamba “Rwebagira “mahali palipotumika kunyongea wahalifu wa makosa ya jinai kama panavyoonekana tokea upande wa pili.

UTARATIBU WA MAZISHI YA OMUKAMA  ALIPOFARIKI.
Chifu (Omukama) wa wanyambo  alipofariki ( hawakutumia neno kuwa kafariki bali walisema ”Omukama yataha”kwa maana ya kwamba amerudi alikotoka) mwili wake ulishonwa kwenye ngozi ya mnyama (Pundamilia) na kuwekwa kwenye mtumbwi ambao ulijazwa maziwa na kupelekwa katika Ziwa Kajunju ambapo alikaa kwenye maji kwa muda wa siku 3 hadi 4 ,wadudu watatu walitolewa katika mwili wake na kukabidhiwa kwa mrithi wake(inasadikiwa kwamba wadudu hawa mmoja aligeuka simba aliyetoa ulinzi kwa Omukama, wa pili chui na tatu fimbo ya utawala)  na baadae mwili ulipekwa makaburini sehemu iliyojulikana kama Kahwela . Hapa mwili uliweka na kujengwa nyumba juu yake ,wasichana 5 na ng’ombe 10 walitolewa kafala ambapo walifungiwa katika nyumba hiyo na kufa kwa njaa . Tendo la mazishi ya Omukama lilijulikana kama ”O’kubyarila”. Shughuli ilifanyika kwa siri sana na ukoo mmoja tu ndio ulihusika na shughuli zote za kuzika mwili mtawala (Omukama ) . Inaaminika ukoo huu ni ule wa ”Abahunga” ,ambao baada ya shughuli hii ya mazishi hawakuruhusiwa kuongea chochote juu ya shughuli hii na kila mmoja alirudi kwake bila kupita tena makao makuu ya mtawala ili wasije kutoa siri.


KUKUA KWA TEKNOLOJIA YA KUFUA CHUMA KATIKA WILAYA YA KARAGWE.   
Wanyambo walikuwa wakijua kufua vyuma (to melt and forge iron ) toka zamani kabla ya utawala wa Wahinda /Wahima katika Karagwe . Waliweza kufua na kuchonga vyuma kutokana na mawe maalum yaliyokuwa yakijulikana kwa lugha ya wenyeji kama “Obutale “(The white stones) . Kazi hii ilikuwa inafanywa na watu wa ukoo wa Abasindi. Na hawa zamani waliishi katika vijiji cha Kibondo, Nyabiyonza karibu na Bweranyange. Makundi mengine ya wafua vyuma yalipatikana katika maeneo ya Nyakabanga, ambayo pia sio mbali sana na Bweranyange .Na pia katika maeneo ya  Igurwa, na Kayanga sehemu za Nsheshe.
Mawe makubwa “Obutale” yaligawanywa na kupondwa katika vipande vidogo vidogo na kuchemshwa kwa moto mkali hadi kuyeyuka. Chuma iliweza kutengenezwa tokana na uji uji ulioyeyushwa na mabaki yaliachwa kupoa yenyewe katika umbo la kifaa kinachotakiwa.  Katika kazi hii waliweza kutengeneza bidhaa kama vile majembe, visu, vijiko, mikuki n.k
Historia inaonyesha kwamba kukua kwa tekinolojia katika Karagwe ilianza miaka mingi iliyopita. Cory (1949;128) akiwanukuu wageni mashuhuri waliwahi kuzuru Karagwe katika karne ya 18 kama T.A. Grant , H.M.Stanley na R.de Z .Hall ;” A Tribal Museum at Bweranyange “ Tanganyika Notes &Records , anasema “ katika nyumba ambayo haitilafiani na nyumba ya kawaida kwa ndani vimewekwa vitu vya kushangaza na kupendeza ambavyo vyaheshimiwa sana na watu wa Karagwe .Navyo ni pamoja na ;-
Ngoma tano zisizo na ngozi ,zilizotengenezwa kwa shaba ; kila moja na mkono wa bangili za chuma zilizofungwa na mikanda na misumari kwenye ngoma .Ngoma mbili zina kimo cha futi mbili na inchi sita kila moja .

Hii ni moja ya mabaki ya ngoma zilizopatikana katika ikulu ya Bweranyange iliyotengenezwa kwa shaba.

Mikuki saba ,ambayo miwili na ina mipini ya chuma na makali ya shaba ,minne mingine ina mipini ya miti na makali ya chuma ; miwili kati ya hiyo ina makali pande nne na moja ina umbo la jembe ,na wa saba ni chuma tupu; mpini wake umetengenezwa kama mlija .


c)    Sampuli nane za chuma zipatazo urefu wa inchi sita mifano ya ng’ombe mmoja zilizogeuzwa chini na watatu wenye nundu.
d)    Magudulia mawili na midumu mingi iliyovunjika iliyotengenezwa Udachi.
Wanyambo wanaamini kuwa Ndagara alileta baadhi ya zana hizi toka Bunyoro na nyingine nyingi alizitengeneza mwenyewe katika shimo alilokuwa akilitumia kwa shughuli ya kufua vyuma. Inasemekana kwamba Omukama Ndagara alifanya kazi yake kwa siri na majira ya usiku. Na aliweza kutengeza baadhi ya vifaa vilivyokuwa vinaonekana Bweranyange kama ilivyoelezwa hapo juu. Ni bahati mbaya sana kwamba alikuwa na usiri sana kiasi kwamba hakuweza kurithisha utalaamu huu kwa watu wengine na inasemekana kuwa hata wale waliokuwa wakimsaidia kazi hii ndani ya shimo aliwapofua macho na wengine kuwauwa ili wasitoe siri ya utalaamu huu.


KUFIFIA KWA UMAARUFU WA UTAWALA WA KARAGWE (The Decline of Karagwe Kingdom).
Inaonyesha kwamba utawala wa Karagwe ulianza kuyumba mara baada ya kifo cha Rumanyika I. Cory (1949; 32- 34) anasema tangu wakati huo historia ya Karagwe imekuwa hafifu na uhafifu huo umekuwa ukiendelea mwaka hadi mwaka. Anaeleza sababu kubwa zilizochangia kuwa kwanza wafalme wote wa wakati huo walikufa wakiwa bado vijana ,na mawakili waliochaguliwa manaibu  wa warithi wao wadogo walikuwa wabaya sana hata yakawepo mabadiliko mengi; pili maradhi mengi yalitokea kwa nguvu sana yaliyoua watu na ng’ombe kwa wingi sana . Mwishoni mwa mwaka 1889 ugonjwa wa sotoka (Rinderpest) uliwaingilia sana ng’ombe katika wilaya ya Karagwe hata mwisho badala ya kuendelea kuwa nchi tajiri sana ya mifugo ikawa maskini.

Jinamizi hili liliwafanya wahima waliokuwa na mifugo ambao walikuwa hawajapata hasara kuikimbia Karagwe wakiwa na mifugo yao kuelekea Kiziba, Kianja na wengine walihamia Rwanda, Burundi na Ankole.

Pia, kufifia kwa umaarufu wa Karagwe ulichangiwa na utawala wa vibaraka waliowekwa na wakoloni mfano Kyobya toka Bukoba na Kaketo toka Bunyoro nchini Uganda. Kyoba aliitawala Karagwe kwa mabavu na majivuno akiwaona Wanyambo kama watu wa chini na wakati mwingine kuwachapa viboko na kuwanyang’anya mifugo yao.

Lakini,hata hivyo wahenga husema “Mnyonge mnyongeni lakini haki yake mpatie” kila mtu anayo mema na mabaya yake , Kyobya atakumbukwa katika  Karagwe  kwa kuingiza zao la Kahawa na ndizi za kupika kwani kabla yake Wanyambo walikuwa wanalima migomba kwa ajili ya kutengezea pombe , hivyo kuingia kwa zao la ndizi kwa ajili ya chakula iliwafanya kujifunza hata upishi wake kwani walizoea ugali wa ulezi tu na nafaka .

10.    HITIMISHO.
Pamoja na changamoto nyingi ambazo zinaikabili zetu (Karagwe na Kyerwa)  na watu wake za kama zile za kijamii, kisiasa, kiuchumi, na kiutamaduni bado ni moja ya wilaya zenye fursa na maliasili nyingi ambazo hazijatumika vizuri.

Katika wilaya zetu za Kyerwa na Karagwe tunayo Mapori manne ya Akiba  za wanyamapori. Mapori hayo ni pamoja Rumanyika Orugundu, Kimisi, Ibanda na Burigi. Mbuga hizi zina wanyama wengi kama vile pofu, nyemera, mamba ,viboko, twiga ,simba, kuro, nyati, tembo na ndege wa aina  wa aina mbali  Mapori haya ya Akiba mbali na kuwa kivutio kwa watalii  na wananchi wanaopenda kuangalia wanyamapori, mito na mabonde;  vile vile hutumika kwa shughuli za uwindaji wa kitalii.  Taarifa kutoka kwa wawindaji bingwa pamoja na Menejimenti ya Pori la Akiba Ibanda inaonesha kuwa kuna densite kubwa ya chui kwenye Pori la Ibanda ikilinganishwa na mapori mengine ya  akiba hapa nchini.

Pori la Akiba Rumanyika ndilo lenye idadi kubwa ya miti ya aina ya Misambya (Markhamia rutia) ambayo inatoa mbao zenye thamani kubwa ukilinganisha na mbao zinazotokana na aina nyingine za miti. Pia , tofauti na mapori mengine ya akiba nchini ,pori hili linasifika kwa kuwa na nyati wafupi (Dwarf Buffalo) .

Aidha, kando kando mwa Pori la Akiba ibanda; yapo maporomoko ya Mto Kagera ambayo kwa sasa serikali za Tanzania na Uganda zimeanza mchakato wa ujenzi ili kufufua mitambo ya umeme iliyoharibiwa wakati wa vita vya Kagera mwaka 1978.
Kivutio kingine katika katika wilaya zetu ni  Msitu wa Hifadhi ya Maji Moto (Mutagata Hot Spring catchment forest ) unaopatikana katika kijiji cha Rwabigaga eneo la Mutagata, kata ya Kamuli ,tarafa ya Kituntu/mabira .Kutoka makao makuu ya wilaya ni umbali wa kilomita 70. Msitu huu ni mdogo wa kijani kibichi muda wote uliotanda miti ya Misambya (Markhamia Lutea) na miti mingine ambayo majina yake hayafahamiki vyema. Katika msitu huu vipo vyanzo vinne vya maji moto, vyanzo hivi ni; (1) Kasiyoza ambacho ni chanzo kikubwa cha maji moto katika eneo hili ambalo maji yake ni nyuzi joto 60-90 ; (2)  Chabakazi ambalo ni eneo dogo linalotoa maji ya moto yenye nyuzi joto 40-60 ; (3) Katagata kake ( hili ni eneo jingine ambalo maji yake ya moto yana nyuzi joto 30-50 na (4) Chandagala chenye maji ya baridi. Historia inaonyesha kwamba chemi chemi hii ilitumiwa na machifu kuogea. Chifu Rumanyika alitembelea eneo hili na kuliwekea Baraka ,akaitukuza chemi  chemi chemi hii na kulitangaza eneo hili kuwa sehemu takatifu na kuanzia wakati huo ,maji hayo hutumika kwa ajili ya tiba ya magonjwa ya ngozi kama vile upele na mapunye ,kifua ,uvimbe wa miguu ,magoti n.k.

Wilaya ya Karagwe na ile ya Kyerwa bado ina ardhi yenye rutuba inayostawisha mazao mengi ya ya kilimo na ufugaji ambayo bado haijatumika ipasavyo. Wakulima wengi katika wilaya hii wanalima kilimo na kufuga kienyeji bila ya kutumia utalaam kuzalisha kwa wingi. Mazao kidogo yanayozalishwa ndio yanasafirishwa kwenda mikoa mingine yanayoifanya Karagwe kusifika. Mazao ya mifugo (Ngozi, maziwa na pembe za ng’ombe) nayo bado hayajatumika vyema, hatuna viwanda vya kusindika mazao haya.

Kila mmoja wetu anajua kuwa wilaya zetu za Karagwe na Kyerwa zinategemea sana kilimo kwa ajili ya chakula na biashara ,lakini mito mingi na mabonde tuliyo nayo haijatumika vyema kuongeza uzalishaji wa chakula . Ili kuinua kipato cha wananchi wa wilaya hizi kuna haja kubwa kwa Halmashauri zetu kutenga bajeti na kuhimiza wananchi kutumia kilimo cha umwagiliaji.

Katika wilaya hii eneo la Kibanda huko Bugomora lilikuwepo shamba la NAFCO na lilikuwa na uwezo wa kuzalisha ngano bora kuliko eneo lolote hapa nchini, eneo hili halitumiki. Tunaweza kufufua shamba hili kama tutakuwa na nia.

Kuhusu namna ya kuhifadhi utamaduni na mila za watu wa Karagwe na Kyerwa hatuna budi kuanzisha makumbusho ya utamaduni wa watu wa Karagwe hapa ,kufufua maeneo ya historia kama vile Bweranyange ,Nyakahanga na Mutagata . Jengo la Nyakahanga linalotumika kwa sasa kama Kituo Kidogo cha Polisi, jengo hili lilikuwa makao makuu ya utawala wa jadi (yaani Olukiko) baada ya kuhamisha mako yake toka kule Bweranyange. Sasa basi ili kutopoteza historia nzuri ya Karagwe tunaomba jengo hili kukarabatiwa bila kubadilisha mfumo wake na kutunzwa vyema kama sehemu ya kumbukumbu ya historia ya utawala wa jadi. Pia, eneo la Bweranyange linatakiwa pia kutunza vyema kama sehemu muhimu ya historia ya watu wa Karagwe

Aidha, hatuna budi kuzienzi na kudumisha mila na desturi nzuri za wanyambo ambazo tayari zimeanza kufifia na kupoteza umaarufu wa kabila hili la wanyambo. Pia, zile mila na desturi mbaya za kibaguzi na zinazowanyanyasa akina mama na zile zenye kurudisha maendeleo nyuma tuachane nazo kabisa.

Tunaomba sherehe hizi za kuadhimisha siku ya utamaduni wa kila kabila kufanyika kila mwaka na Halmashauri zetu kutenga bajeti ya kutosha kufanisha lengo hili.


Mwisho, naomba kutoa wito kwamba Karagwe na Kyerwa yenye maendeleo inawezekana iwapo tutakuwa na mshikamano wa pamoja katika kuhifadhi maeneo ya kihistoria pamoja na kuendeleza mila nzuri za kabila hili. Kwa maana taifa lisilokuwa na utamaduni wake ni sawa na taifa lililokufa. Ni ukweli usipingika hata nchi zote zilizoendelea bado wametunza na wanaendeleza maeneo ya kumbukumbu ya kihistoria kwa ajili ya utalii na pia kwa faida ya vizazi vijavyo.
Imeandaliwa na


Livingstone Byekwaso
Mratibu –SAWAKA 
0754 894 537Thursday, 23 May 2013

UTAMADUNI WA WANYAMBO WA KARAGWE NA KYERWA MKOANI KAGERA Na Tumaini Anathory-Karagwe

BAADHI YA VYOMBO ASILIA VYA MNYAMBO (ORUGUNDA, ENKAYE NE'BISISI). BADALA YA VYOMBO HIVI,SASA NI MADUMU, GLASI, JAGI NA SUFURIA

MADAWA ASILIA YA KABILA LA MNYAMBO

BAADHI YA VYOMBO  VYA WANYAMBO PAMOJA NA VYAKULA ASILIA(ESWIGA,AMATECHE,AMASOMA NE ESOJE)
Wednesday, 22 May 2013

WANYAMBO SIO WAHAYA KAMA INAVYOSADIKIKA-


Na Tumaini Anathory  Karagwe-Kagera.
Moja ya ngoma asilia za wanyambo wa Karagwe- Amakondere.


Tamasha la utamaduni wa Kabila la Wanyambo waishio katikaWilaya za Karagwe na Kyerwa Mkoani Kagera, limeshuhudia maelfu ya washiriki kutoka maeneo mbalimbali ya Wilaya hizo kutoka kwa mwenzake kuhusiana na mila na desturi asilia za kabila hilo ,mila zao  ambazo zinazidi kutoweka kila uchao, kutokana na  kile kinachoelezwa kuwa ni kuenea kwa Teknolojia mpya zinazoibuka zikieneza  tamaduni za kigeni kutoka maeneo mengine hasa kutoka nchi za ughaibuni.Kubwa zaidi wanyambo walikuwa na hamu ya kujua ni kwa nini kabila lao linafananishwa na lile la ndugu zao Wahaya kutoka Bukoba.

Taasisi zinazojishughulisha na uhamasishaji wa utamaduni asilia,vikundi vya ngoma asilia vya vijana na wazee,wakishirikishwa watoto kwa uchache,wakiongozwa na shirika la SAWAKA ambalo limeshiriki kuratibu Tamasha hilo Wilaya za Karagwe na Kyerwa,walijimwaga katika uwanja wa mpira wa miguu mjini Kayanga Mei .21. 2013 ambako lilifanyika tamasha hilo, likizihusisha Wilaya hizo mbili ambazo asili yake ni moja kwa kuunganishwa na kabila moja la Wanyambo wote wakijitahidi kutetea kabila hilo.

Akisoma Historia ya Karagwe tangu enzi za utawala wa Wakama, historia iliyosheheni chimbuko la kabila hili  ambalo kiukweli limefichika ndani ya Kabila la wahaya, ukiuliza kabila la mkazi wa Karagwe nje ya mkoa wa Kagera kwa walio wengi, Mratibu wa Shirika la SAIDIA WAZEE KARAGWE (SAWAKA)ambaye pia ni Katibu Mkuu wa Shirika la KARAGWE MEDIA ASSOCIATION (KAMEA)Shirika ambalo ni mmiliki wa Radio Karagwe FM Bw.Livingiston Byekwaso amesema kuwa,asili ya jina Karagwe kutokana na simulizi za wazee mbalimbali na watafiti wa historia ya Karagwe akiwemo Profesa Katoke katika kitabu chake alichokitunga mwaka 1975,inaelezwa kuwa ,jina hili lilitokana na kilima kilichoko kusini Magharibi mwa makao makuu ya Wilaya ya Karagwe kwenye kijiji cha Kandegesho Kata ya Nyakakika mahali ambako Mukama wa Kwanza Nono ya Marija alifanyia kafara ya kwanza.

Akiendelea kuelezea umuhimu wa kuuenzi utamaduni wa mnyambo ambao umekuwa haujulikani, Byekwaso alisema.“ Kwa tafsiri yangu napenda kuamini kwamba,wakoloni kwa sababu ya kurahisisha utawala walilinganisha wanyambo toka Karagwe na Wahaya kutoka Bukoba na wote kuitwa Wahaya, ili kurahisisha utawala wao walipoingia hapa nchini.Lakini ni ukweli usiopingika kwamba wanyambo wanapatikana katika Wilaya ya Karagwe na wahaya kutoka Bukoba wanatofautiana sana kutokana na asili yao,shughuli za kiuchumi,kijamii,mila na desturi,mazingira na lugha zao”.

Akiwahutubia washiriki wa Tamasha hilo,mgeni rasmi ambaye alikuwa ni Katibu Tawala wa Wilaya ya Karagwe Mustafa Said alisema kuwa,Utandawa umekuwa changamoto kubwa ambapo vijana walio wengi wamejikita katika mitandao ya kijamii kama vile facebook ,twitter na mitandao ya kisasa jambo ambalo limechangia kwa kiasi kikubwa kusababisha mmomonyoko wa maadili ya utamaduni asilia.Saidi aliwataka vijana kuwa makini na matumizi ya utandawazi kwani utandawazi huo ukitumika vibaya,madhara yake ni makubwa.Aidha aliwataka wana Karagwe kuziepuka mila na desturi potofu hasa tabia za wanaume kuwachapa viboko wanawake zao.

Tamasha hili ni la pili baada ya lile le kwanza lililofanyika Katika Kijiji cha Makumbusho Jijini Dar es salaam mwaka 2011 ambapo Tamasha la utamaduni kitaifa liliwakilishwa na kabila la Wanyambo wakiwa kama washiriki katika tamasha hilo kwa mara ya kwanza.      
  
Wednesday, 15 May 2013

EDITED ADVERT:JOB OPPORTUNITIES ADVERTISEMENTKaragwe Media Association (KAMEA) is a Non –partisan, Non-discriminatory, Non –Governmental voluntary organization based in Karagwe District of the United Republic of Tanzania .The organization is registered with the Ministry of Home Affairs under rule 5 of the society’s ordinance of 1954, with certificate SO No.11023 of 31st August 2001. KAMEA’s mission is to fill in the communication gap for the stimulation of social, economic, and cultural development through education, information provision and linking the Karagwe community in various social sectors. Karagwe Media Association (KAMEA) is urgently looking for suitable candidates to fill in the following post:-

RADIO MANAGER ( 1 POST)

The radio manager shall be employed by the Radio Board

The responsibilities of the radio manager are

1. To implement the decisions of the Radio Board

2. To report to the Radio Board

3. To secure that the policies regarding content decided by the Radio Board are implemented

4. To represent the radio board in national networks

5. Together with the chairperson of the board to sign contracts with customers

6. To identify candidates for vacant posts and present these to the Radio Board

7. To facilitate the daily works at the radio

8. To overview the daily bookkeeping

9. To receive visitors

10. The radio manager shall be the secretary to the board and arrange the meetings after making consultations with the chairperson.

11. To write monthly and annual progress reports of the radio station.

Requirements

i) Be a Tanzanian citizen,

ii) Age of (25- 40 years )

iii) Experience with radio management or any other related field for at least one year,

iv) Having a Bachelors degree in Mass Communication or Advanced Diploma in Journalism and or Community Development
v) Self initiated and motivated.

All application should be sent to:

General Secretary, Karagwe Media Association (KAMEA)

P.O.Box 316 Karagwe-Kagera Tanzania

Email:kcrp.phase2@gmail.com or byekwaso2005@yahoo.com

Mob: +255 752 093 512 +255 789 870 311 +255 754 894 537 OR

Radio Karagwe FM, Sauti ya Wananchi

P.O.Box 316 Karagwe

Email: karagwefmradio@yahoo.com Mob: + 255 757 222 255 +255 785 551 522

Deadline for all applications is 30th, June, 2013 at 16:30

Tuesday, 14 May 2013

Polisi Mkoani Kagera yakamata Watu wanane wanaosadikiwa kuwa ni Majambazi Sugu.


Bunduki moja aina ya SMG na risasi 16 iliyokamatwa na jeshi la Polisi Mkoani Kagera.

Kaimu Kamanda wa polisi mkoa wa Kagera Henry Mwaibambe akionyesha bunduki na risasi zilizokamatwa.


Polisi mkoani Kagera wamewakamata watu wanane wanaosadikiwa kuwa ni majambazi sugu, ambao wamekuwa wakitafutwa kwa tuhuma za kuhusika na matukio mbalimbali ya uhalifu ikiwemo utekaji wa magari maeneo ya porini na uporaji wa mali za wafanyabiashara.
Kaimu Kamanda wa polisi mkoa wa Kagera Henry Mwaibambe anasema kwa muda mrefu polisi wamekuwa wakifuatilia mtandao wa majambazi wanaojificha katika mapori, ambapo huteka magari na kupora mali za wafanyabiashara.
Anawataja waliokamatwa kuwa ni pamoja na mwanamke mmoja Leoncia Rovast (28), ambaye anadaiwa kuwa kinara wa kupanga mipango ya utekaji na uporaji.
Watuhumiwa wengine kuwa ni Iman Ezekiel (24), Ndanda Iliofu (24), Hanana Francis A.KA Baseka (26) Kabichi Sylivestar (23), Slambuki Abel (25) na Amos Amos (30) A.K.A Rasi.
Wengine ni Sabuhalo Daud (26) ambaye anatuhumiwa kuhusika na utunzaji wa mali na vifaa vinavyoporwa baada ya utekaji, ambapo alikutwa na bunduki moja aina ya SMG na risasi 16.

ARDHI YA NYAKASIMBI YARUDISHWA MIKONONI MWA WANAKIJIJI.
Na Tumaini Anathory
KARAGWE-KAGERA

Mkuu wa Wilaya ya Karagwe mkoani Kagera (katikati) 

 M
kuu wa Wilaya ya Karagwe Bi.Darry Rwegasira ametoa tamko rasmi kuhusu nani mmiliki halali wa ardhi katika mgogoro uliodumu kwa zaidi ya mwaka mmoja kati ya wanakijiji cha Nyakasimbi Wilayani Karagwe pamoja na mwekezaji anayedaiwa kuwa mhamiaji haramu kutoka nje ya Tanzania.
Bi.Rwegasira alitoa tamko kuwa ardhi ile ni mali ya wanakijiji cha Nyakasimbi kata ya Nyakasimbi kupitia mkutano wa hadhara wa wananchi kijijini hapo Mei. 14. 2013 baada ya tume aliyoiunda mapema mwaka jana kuchunguza swala hilo, kukamilisha kazi yake ambapo amesema kuwa, pamoja na mambo mengine yaliyobainiwa na tume yake ugawaji wa ardhi hiyo kwa mwekezaji huyo ulikiuka  taratibu za ugawaji ardhi kisheria.
Aidha mkuu huyo wa Wilaya aliuagiza uongozi wa Kijiji hicho kupitia upya taratibu za kisheria kuhusu matumizi bora ya Ardhi na kugawa upya eneo hilo kwa wanakijiji  watakaoomba ardhi wakizingatia maelekezo ya sheria ili kuepuka migogoro mingine kama ile ambayo imesababisha hali ya kutoelewana baina ya uongozi wa kijiji pamoja na wanakijiji.
Hata hivyo Bi.Rwegasira ameongeza kuwa watendaji wote waliohusika kugawa holela ardhi hiyo bila kufuata taratibu,watachukuliwa hatua za kisheria ikiwa hatua hiyo inafuatia hatua kali ambazo zimeshachukuliwa dhidi ya viongozi waliokuwa wakidaiwa kuwabeba wale ambao wanadaiwa kuiteka ardhi hiyo kwa minajiri ya ufugaji kinyume cha sheria.
Itakumbukwa kuwa, hivi karibuni Waziri wa mambo ya ndani ya nchi Dk Emmanuel Nchimbi alimfukuza kazi  Mrakibu Mwandamizi wa Polisi, Peter Matagi aliyekuwa Mkuu wa Upelelezi wa Mkoa wa Kagera akituhumiwa kuwapiga na kuwabambikizia kesi zisizo na dhamana wananchi wa kijiji cha Nyakasimbi ambao walikuwa wakidai kupokonywa ardhi yao na wafugaji wanaodaiwa kutokuwa raia wa Tanzania.
Akielezea uamuzi huo wa kumfukuza kazi ofisa huyo,Waziri nchimbi alisema, “Mwaka jana kulikuwa na mgogoro wa ardhi katika Kijiji cha Nyakasimbi huko Kagera kati ya wanakijiji na mmiliki mmoja wa shamba, wananchi waliona kuwa mmiliki wa shamba hilo ana eneo kubwa hivyo walikubaliana katika mkutano wa kijiji kuingia kwenye shamba hilo kwa nguvu,” alisema Dk Nchimbi na kuongeza:
“Waliingia na kuanza kuswaga ng’ombe kuelekea kwa Mkuu wa Wilaya, walikamatwa watu 12 lakini wawili walifanikiwa kutoroka na walisafiri hadi Dodoma kumwona mbunge wao, ambaye aliomba kuonana na mimi.”
Dk Nchimbi alisema licha ya kukubali kuonana nao,  ilishindikana baada ya watu hao kukamatwa wakidaiwa kuwa ni majambazi ambao walikuwa wakitafutwa huko Karagwe.
“Nilimpigia simu Kamanda wa Polisi Kagera nikitaka kuonana na hao majambazi katika Hoteli ya Dodoma na waliletwa na niliwasikiliza na kugundua kuna tatizo la wao kubambikiziwa kesi ya ujambazi wa kutumia silaha ambayo huwa haina dhamana,” alisema.
Alisema aliunda timu ambayo aliiongoza akiwa na Naibu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA), Aggrey Mwanri na Naibu Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Goodluck Ole Medeye na kusimamia uchunguzi na Ofisi ya Mwanasheria wa Serikali iligundua hakuna mashtaka kama hayo na ndiyo maana Matagi anafukuzwa kazi na kushtakiwa kijeshi.